Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Yair Golan, kiongozi wa chama kinachoitwa “Democrats” ndani ya utawala wa Kizayuni, alisema:
“Kutambua nchi ya Palestina ni hatari kubwa kwa usalama wa Israel na ni fedheha ya kisiasa kwa Netanyahu na Smotrich.”
Kwa upande wake, Miki Zohar, Waziri wa Utamaduni na Michezo wa utawala huo, alisema:
“Kutambua Palestina haina maana yoyote na ni dalili ya chuki dhidi ya Wayahudi na chuki kwa Israel. Jibu pekee la hatua hii ni kuimarisha utawala wa Israel katika Ukingo wa Magharibi.”
Aidha, Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani, alidai kuwa hatua ya Uingereza, Australia na Canada ni “zawadi kwa wauaji” na akataka hatua za haraka za kulipiza kisasi, akisisitiza:
“Ni lazima tuimarishe utawala wetu mara moja katika Ukingo wa Magharibi na kuiondoa kabisa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel pia ilidai kwamba viongozi wa Hamas wamekiri wazi kuwa kutambuliwa kwa Palestina ni matokeo ya tukio la Oktoba 7.
Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha, alisema:
“Siku ambazo Uingereza na mataifa mengine yalikuwa yakiamua mustakabali wetu zimekwisha. Jibu pekee ni kuimarisha utawala wetu katika Ukingo wa Magharibi.”
Hatua ya kihistoria ya kutambua Palestina
Serikali ya Uingereza siku ya Jumapili (30 Shahrivar 1404) sambamba na Australia na Canada, ilitangaza rasmi kutambua nchi huru ya Palestina — hatua ya kihistoria inayoashiria mpasuko unaoongezeka kati ya Magharibi na utawala wa Kizayuni.
Uingereza awali ilishatoa onyo kwamba iwapo Israel haitachukua hatua madhubuti kumaliza mgogoro wa kibinadamu Gaza, London itaitambua Palestina katika muktadha wa kulinda kile walichokiita “suluhisho la mataifa mawili.”
Masharti yaliyotajwa na Uingereza ni pamoja na:
- Kusitisha mara moja mashambulizi ya Israel na kukubali kusitishwa kwa mapigano,
- Kuhakikisha amani ya kudumu na kufufua mtazamo wa suluhisho la mataifa mawili,
- Kutoa ruhusa kwa Umoja wa Mataifa kuendelea na misaada ya kibinadamu,
- Kuepuka kuendelea na ukaliaji wa mabavu katika Ukingo wa Magharibi.
London imesema kuwa hakuna mojawapo ya masharti haya yaliyotekelezwa, na mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya Qatar yamefanya hali ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kuwa ngumu zaidi.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema kuwa nchi yake imeitambua Palestina “ili kufufua matumaini ya amani.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney alisema kuwa hatua ya Ottawa ni utekelezaji wa ahadi yake ya muda mrefu ya tangu mwaka 1947, huku akisisitiza msimamo wa Canada wa kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili. Hata hivyo, bila kugusia jinai za Kizayuni tangu 1948, alisisitiza kuwa Hamas ni “shirika la kigaidi.”
Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese naye pia alitangaza kuwa taifa lake “linatambua rasmi nchi huru ya Palestina yenye mamlaka kamili.”
Aliongeza kuwa hatua hii imefanyika kwa ushirikiano na Canada na Uingereza, akisema:
“Uamuzi huu ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kurahisisha utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili — ambalo daima limekuwa njia pekee ya amani na usalama wa kudumu kwa Israel na Palestina.”
Your Comment